Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uingereza yatoa msaada kwa FAO kunusuru waathiriwa wa mzozo Sudani Kusini

Uingereza yatoa msaada kwa FAO kunusuru waathiriwa wa mzozo Sudani Kusini

Shirika la Chakula na Kilimo duniani, FAO limeungwa  mkono harakati zake na Serikali ya Uingereza kwa kupatiwa msaada wa zaidi ya dola milioni 13 ili kusaidia familia zilizoathiriwa na mgogoro nchini Sudani Kusini, kufufua kilimo na kujikwamua katika ukosefu wa chakula unaoandama taifa hilo. Taarifa zaidi na Alice Kariuki

(Taarifa ya Alice)

FAO inasema kuwa zaidi ya watu milioni saba wapo hatarini kukubwa na njaa na imehimiza kuchukuliwa kwa hatua za haraka ili kukabiliana na tishio hilo.

Kiasi hicho cha watu kimejumuisha pia wale milioni moja ambao wamekimbia makazi yao kutokana na machafuko yanayoendelea.

Inaripotiwa kuwa mifugo zaidi ya milioni kumi imeondolewa kwenye maeneo yao ya malisho na hivyo kuvuruga shughuli zote za kilimo.

FAO imesema kuwa msaada huo uliotolewa na Uingereza umekuja wakati mwafaka ikiwa ni muhimu shughuli za kusambaza mbegu hizo ziendelee kabla ya msimu wa mvua unaotarajiwa kuanza muda usio mrefu. Mkurugenzi wa kitengo cha misaada ya dharura Dominique Burgeon anaeleza umuhimu wa msaada.