Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa Palestina watapata haki, asema Mkuu wa UNRWA aneyendoka

Wakimbizi wa Palestina watapata haki, asema Mkuu wa UNRWA aneyendoka

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwasaidia Wakimbizi wa Kipalestina, Filippo Grandi, amesema kuwa wakimbizi wa Kipalestina watakuja kupata haki yao hatimaye, wakati akihitimisha muhula wake wa kuhudumu katika wadhafa huo, ambao unamalizika kesho Machi 29.

Bwana Grandi, ambaye ni raia wa Italia, anaukabidhi wadhfa huo wa kuisimamia UNRWA kwa Bwana Pierre Krahenbuhl, raia wa Uswisi. Bwana Grandi alijiunga na UNRWA mnamo Oktoba 2005 kama Naibu Kamishna Mkuu, na kuchukuwa wadhfa wa kuliongoza shirika hilo mnamo Januari 2010.

Wakati wa muhula wake katika ofisi hiyo, kulishuhudiwa matatizo makuu kwa wakimbizi wa Palestina, yakiwemo vita vya Lebanon mwaka 2006, uharibifu wa kambi ya wakimbizi ya Nahr el-Bared nchini Lebanon mwaka 2007, mapigano ya Gaza kuanzia 2007-2009, na Novemba 2012, na pia mgogoro wa Syria.