Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wajumbe wa Baraza Kuu waendelea kuchangia rasimu ya azimio kuhusu uzingatiaji wa mipaka ya Ukraine

Wajumbe wa Baraza Kuu waendelea kuchangia rasimu ya azimio kuhusu uzingatiaji wa mipaka ya Ukraine

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linaendelea na kikao cha wazi kikiangazia kuzuia majanga ya kivita, kwa kuimarisha dhima ya usuluhishi kwa kutatua migogoro kwa njia ya amani.

Katika kikao hicho imewasilishwa rasimu ya azimio kuhusu uzingatiaji mipaka ya Ukraine ikitajwa kuwa hivi karibuni mipaka ya nchi hiyo imeingiliwa na nchi nyingine.

Azimio hilo linaeleza bayana kuwa kura ya maoni iliyofanyika Crimea tarehe 16 mwezi huu haina uhalali wowote na haiwezi kuwa msingi wa kubadilisha hadhi ya jamhuri inayojitawala ya Crimea au jiji la Sevastopol.

Kwa mantiki hiyo azimio hilo linataka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na mashirika yake kutotambua mabadiliko yoyote ya hadhi ya Crimea na mji huo kwa msingi wa kura hiyo ya maoni na kujizuia kuchukua hatua yoyote inayoweza kutafsiriwa utambuzi wa mabadiliko ya hadhi hiyo.

Wajumbe hivi sasa wanachangia rasimu hiyo ambapo Mwakilishi wa Ukraine amepinga atua ya Urusi kujimegea ardhi yake, huku Urusi ikisema kuwa kura ya maoni Crimea imefanyika kihalali.

Muungano wa Ulaya umesema hauitambui na kutaka Urusi kujiondoa huku ukiunga mkono mazungumzo kati ya viongozi wa Urusi na Ukraine hivi karibuni na hatua ya Umoja wa Mataifa kupeleka jopo la kuchunguza haki za binadamu.

China imesema haipendi kinachoendelea Ukraine na kunatakiwa mizania katika kupatia suluhu kinachoendelea. Hata hivyo imesema upigiaji kura rasimu hiyo utazidi kuchochea hali ya sasa.

Japan kwa upande wake imesema inapinga kinachoendelea na itapiga kura kuunga mkono rasimu ya azimio hilo kuonyesha msimamo wake wa kupinga kuingiliwa kwa mipaka ya Ukraine.