Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanajeshi 20 wauawa Yemen: UM walaani

Wanajeshi 20 wauawa Yemen: UM walaani

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani vikali shambulio lililotokea sehemu ya Hadramawt, Yemen, lililosababisha wajeshi 20 kupoteza uhai. Baraza lilirejelea wito kwa nchi zote za Umoja wa Mataifa kushirikiana na serikali ya Yemen ili watekelezaji wa tukio hilo wahukumiwe.

Wanachama wote wa Baraza la Usalama wamepeleka rambirambi zao kwa familia za wahanga wa shambulio hilo, amesema Sylvie Lucas, ambaye ni mwakilishi wa kudumu wa Luxembourg, na raisi wa baraza kwa mwezi huu. Baraza la Usalama pia limesisitiza kwamba ugaidi unatishia usalama na amani duniani, katika muktadha wa  mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Awali, wanachama wa baraza la usalama wametaka kukumbusha serikali zilizochukua hatua ya kupambana na ugaidi, kwamba zinapaswa kuheshimu sheria za kimataifa, hasa haki za binadamu.