Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sierra Leone tumeimarika sasa tunasonga mbele: Waziri Kamara

Sierra Leone tumeimarika sasa tunasonga mbele: Waziri Kamara

Safari ya miaka 15 ya Umoja wa Mataifa kusaidia ujenzi wa amani nchini Sierra Leone baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe imefikia ukingoni mwishoni mwa mwezi huu na hii leo Baraza la Usalama limepokea ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu majukumu yaliyotokelewa na changamoto zilizobakia baada ya hatua hiyo.

Mathalani ripoti hiyo inataja mafanikio yaliyopatikana miaka 12 tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe kuwa ni pamoja na kuendelea kujikwamua kutoka madhara ya vita na chaguzi tatu za kidemokrasia zilizofanyika kwa amani.

Hata hivyo ripoti hiyo inasema hatua za makusudi zinapaswa kuchukuliwa ili kulinda mafanikio hayo.

Miongoni mwa walioshiriki kikao hicho cha baraza la usalama ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Sierra Leone Samura Kamara ambaye amewaeleza waandishi wa habari kuwa wana shukrani nyingi kwa Umoja wa Mataifa na jumuiya ya kimataifa kwani kwa juhudi zao nchi yake sasa ina mengi ya kujivunia..

(Sauti ya Waziri Kamara)

Leo tumebadilika kwa mafanikio makubwa kutoka nchi inayopokea walinda amani wengi zaidi hadi kuwa nchi inayopeleka walinda amani nchi zingine, lakini pia nchi ambayo tunaamini inajaribu kwa uwezo wake wote kushughulikia chanzo kilicholeta mgogoro Sierra Leone.”

Waziri Kamara amesema msingi wa mafanikio yao ni kujumuisha wananchi wote wa Sierra Leone hata wale wanaoishiughaibuni, katika michakato inayoendelea kwenye nchi yao na kujikosoa ili kubadili mitazamo isiyokuwa na msingi wa maendeleo.

Tangu mwaka 1998 Umoja wa Mataifa umekuwa na ofisi zake nchini Sierra Leone zilizokuwa zinabadili majukumu kuanzia yale ya uangalizi, UNOMSIL, ujumbe kamili-UNAMSIL na ofisi jumuishi ya ujenzi wa amani UNPSIL mwaka 2008 ambayoshughuli zake zimefungwa rasmi mwezi huu.

Kinachofuatia sasa ni Umoja wa Mataifa kufungua ofisi ya mwakilishi wake nchini Sierra Leone.