Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban alaani mauaji ya mlinzi kutoka Iran

Ban alaani mauaji ya mlinzi kutoka Iran

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani vikali mauaji ya mlinzi wa mpaka kutoka Iran na kundi la wanamgambo. Mlinzi huyo alikuwa mmoja wa walinzi watano ambao walitekwa nyara na kundi hilo kusini mashariki mwa mpaka mapema mwezi Februari.

Katika taarifa iliotolewa na msemaji wake Katibu Mkuu ameelezea mshikamano wake na serikali na watu wa Iran.

Ametaja mauaji hayo kama kitendo kibaya ambacho kilitendeka wakati sherehe za maadhimisho ya mwaka mpya, Nowruz zikiendelea.

Ban ametoa wito kwamba waliotekeleza kitendo hicho wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria huku akituma salamu za rambirambi kwa familia ya mlinzi huyo na kuongeza kuwa ni matumaini yake kwamba Serikali ya Iran itapata ushindi wa kuachiwa huru kwa walinzi hao wanne.