Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamisheni kusaidia mchakato wa mpito wa ofisi ya UM Burundi

Kamisheni kusaidia mchakato wa mpito wa ofisi ya UM Burundi

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao cha wazi kuhusu utendaji wa Kamisheni ya umoja huo kuhusu ujenzi wa amani yenye jukumu la kuratibu ofisi za ujenzi wa amani kwenye maeneo baada ya mizozo. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi:

(Taarifa ya Assumpta)

Katika kikao hicho, wajumbe walisomewa ripoti ya utendaji ya kamisheni hiyo kwa kipindi cha Januari Mosi hadi Disemba 31 mwaka 2013 ikiangazia yaliyojiri, changamoto na mwelekeo wa baadaye.

Mwenyekiti wa zamani wa kamisheni hiyo, Balozi Ranko Vilovic wa Croatia amesema wamesaidia mchakato wa mpito wa ofisi ya ujenzi wa amani Sierra Leone, UNIPSIL jambo ambalo baraza la usalama linahitimisha huku wakijiandaa kusaidia mchakato wa aina hiyo Burundi.

(Sauti ya Balozi Vilovic)

“Baraza la usalama linahitimisha uamuzi wa kufunga UNIPSIL na hivyo kuashiria Sierra Leone katika zama mpya ya mabadiliko yake kwenye maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Mwaka huu tume itajikita kusaidia hatua nyingine iliyopangwa ya mpito wa ofisi ya Umoja wa Mataifa Burundi.”

Balozi Vilovic amesema katika mchakato huo, mambo ambayo kamisheni imejifunza kwenye kuboresha ofisi hizo za ujenzi wa amani yatatumika kama mifano ya kuimarisha kazi zake na hata ofisi za uwakilishi wa Umoja wa Mataifa zitakazofunguliwa.

Kwa sasa kamisheni hiyo inasimamia ofisi za Umoja wa Mataifa za ujenzi wa amani, Ukanda wa Afrika Magharbi, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Liberia, Sierra Leone na Guinea-Bissau.