Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa Panyabuku waleta ustawi kwa wanawake China

Mradi wa Panyabuku waleta ustawi kwa wanawake China

Maisha ya wanawake maskini kwenye maeneo ya vijijini nchini China yamebadilika na kuwa bora kutokana na mradi wa ufugaji panyabuku ulioratibiwa na Shirika la kimataifa la maendeleo ya kilimo, IFAD.

Kupitia mradi huo wanawake hao walipatiwa stadi za ufugaji wanyama hao ambao ni kitoweo cha hali ya juu nchini China.

IFAD inasema mradi ulianza mwaka 2002 ukijumuisha vijiji 10,000 jimbo la Guangxi na kufikia wakulima 900,000 asilimia 60 wakiwa wanawake.

Miongoni mwao ni Cai'Mei Zhao ambaye amesema kupitia mradi huo alitembelea nchi mbali mbali kuona ufugaji wa panyabuku na alipata mkopo wa dola 800 kuanzisha mradi.

Anasema licha ya changamoto kama vile magonjwa ya wanyama na ukosefu wa soko hapo awali, sasa ameweza kuboresha maisha ya familia na jamii yake mathalani kugharimia elimu na makazi kwani amepata soko kwenye migahawa na maduka makubwa.

IFAD ilifunga mpango wa usaidizi mwaka 2008 ambapo takwimu zimeonyesha kuwa idadi ya kaya zilizokuwa kwenye umaskini wa kupindukia katika eneo hilo ilipungua kwa theluthi moja kutoka 129,000 hadi 41,700.

Hata hivyo Zhao ameweza kufungua chama cha ushirika cha wanawake cha kufuga panyabuku kikiwa na wanachama kutoka wilaya na majimbo mbali mbali.