UNSOM yalaani mauaji ya viongozi wa kaya Somalia

25 Machi 2014

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu nchini Somalia, Nicholas Kay, amelaani vikali mauaji ya viongozi wa kaya wanane pamoja na mashumbulizi kati ya vikundi tofauti vinavyodai kuwakilisha serikali, yaliyotokea jana Baidoa, kusini mwa Somalia. Ametuma rambirambi zake kwa familia na jamii za waliouawa akisisitiza umuhimu wa uchunguzi ili waliotekeleza uhalifu huo wahukumiwe ipasavyo.

Kwa mujibu wa Serikali ya Muungano wa Somalia, viongozi hao wanane waliviziwa na kuuawa na Al-Shabaab wakiwa wanahudhuria kikao cha kujenga nchi.

Akizungumza mbele ya Baraza la Usalama na Amani la Muungano wa Afrika, Bwana Kay ameiomba serikali ya Somalia isimamie taratibu za kulinda amani na kujenga nchi.

Alikaribisha azimio la serikali kuanzisha mazungumzo na viongozi mbali mbali bila kuchelewa, akiongeza kwamba ofisi ya umoja wa mataifa Somalia, UNSOM, itaendelea kusaidia serikali ya Somalia, kwa kushirikiana na Ofisi ya Muungano wa Afrika nchini Somalia, AMISOM, IGAD, na Muungano wa Ulaya, katika jitihada zake za ujenzi wa nchi.