Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan na Sudan Kusini sasa zimesahaulika, watoto wahoji matunda ya uhuru: Ging

Sudan na Sudan Kusini sasa zimesahaulika, watoto wahoji matunda ya uhuru: Ging

Kadri mizozo na majanga yanavyozidi kuibuka maeneo mengine duniani, mustakhbali wa wakazi wa Darfur huko Sudan unazidi kutoweka huku nchini Sudan Kusini watoto wanahoji yalikoenda matarajio ya matunda ya uhuru wa taifa lao changa.

Hayo ni miongoni mwa mambo yaliyosemwa na viongozi wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na usaidizi wa kibinadamu, OCHA walipozungumza na waandishi wa habari mjini New York, kuhusu ziara yao kwenye nchi mbili hizo, ziara iliyohusisha jopo la wakurugenzi kutoka chombo cha ubia cha masuala ya dharura baina ya Umoja huo na mashirika ya kiraia.

John Ging ambaye ni Mkuu wa operesheni ndani ya OCHA amesema mizozo inayoibuka imeathiri kiwango cha usaidizi wa fedha huko Sudan licha ya kwamba mahitaji yanaongezeka kila siku kutokana na wananchi kukimbia makazi yao kwa sababu ya mapigano.

(Sauti ya John Ging)

"Mwaka 2011 tulikuwa na asilimia 65 ya ombi letu, mwaka 2013 ilipungua hadi asilimia 57 na mwaka huu inasikitisha zaidi kwani tumepata asilimia Tatu tu ya dola Milioni 995 tuliozoomba.”

Yasmine Haque, Naibu Mkurugenzi wa operesheni OCHA akagusia Sudan Kusini ambapo anasema hali sasa inasikitisha tofauti na matarajio ya watoto walipoulizwa matarajio yao punde baada ya uhuru mwaka 2011.

(Sauti ya Yasmine Haque)

Walitaka amani, ulinzi na elimu, na chakuhuzunisha kwa watoto wengi Sudan Kusini hilo si jambo la uhalisia, na ni vigumu sana kusema ni lini ndoto yao hiyo inaweza kuwa ya matumaini.”