Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM na wadau waendelea na usaidizi wa kiutu kwa wakimbizi wa Syria

UM na wadau waendelea na usaidizi wa kiutu kwa wakimbizi wa Syria

Umoja wa Mataifa na wadau wake wameendelea kutoa usaidizi kwa wananchi wa Syria wanaoendelea kukumbwa na madhila kufuatia mapigano yanayoendelea nchini mwao huu ukiwa ni mwaka wa nne sasa.

Umoja huo kupitia ofisi yake ya kuratibu misaada ya kiutu, OCHA leo umetangaza kuwa malori 12 hatimaye yameweza kuingia Syria kutoka Uturuki yakiwa yamesheheni vyakula na vifaa vingine kama vile vya matibabu.

Msafara huo unaelekea eneo la Al Hasakeh ambapo OCHA inatoa wito kwa uwezeshaji wa malori mengi zaidi kupitishwa mpakani hapo ili kuongeza usaidizi kwa wahitaji.

Msafara mwingine wa malori 16 ukiwa na vifaa vya kukidhi mahitaji ya familia ikiwemo mablanteki umeingia Syria kwa mujibu wa UNICEF na utanufaisha watu Elfu 25.

Wakati huo huo shirika la kimataifa la uhamiaji, IOM limesema wiki hii limevuka kiwango chake cha kusafirisha wakimbizi 400,000 wa Syria kwenda katika kambi zilizo nchini Jordan.