Mkurupuko wa Ebola Guinea-Conakry waua watu 59, WHO, EU yasaidia uchunguzi na tiba

25 Machi 2014

Shirika la afya duniani WHO limesema watu 59 wamefariki dunia kutoka na ugonjwa wa Ebola huko Guinea-Conakry, huku likitanabaisha kuwa uchunguzi dhidi ya watu waliokuwa wanashukiwa kuwa na ugonjwa huo huko Canada umebaini kuwa si Ebola. Taarifa zaidi na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Sintofahamu ya kuibuka kwa ugonjwa huo imeibuka mwishoni mwa wiki ambapo waliothibitika kufariki dunia kutokana na Ebola ni miongoni mwa visa 86 vilivyokuwa vimeripotiwa. WHO inasema wagonjwa hao walibainika kwenye maeneo ya misituni yaliyo kusini mwa Guinea karibu na mpaka wa Sierra Leone na Liberia. Kinachofanyika sasa ni kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo wenye kiwango cha juu cha kuambukiza. Tarik Jasarevic ni msemaji wa WHO Geneva.

(Sauti ya Tarik)

“Huko Gekedu, madaktari wasio na mpaka kutoka Uswisi wametenga wodi maalum ya wagonjwa wa Ebola kwenye hospitali ambako pia Muungano wa Ulaya kupitia WHO imepeleka maabara maalum kusaidia uchunguzi. Wagonjwa wawili Conakry wamebainika hawana virusi vya Ebola. Jumla tuna Visa 13 vilivyothibitishwa kwenye maabara. WHO pia inapeleka wataalamu mbali mbali wa tiba ikiwemowale wa kudhibiti magonjwa ya milipuko.”

Dalili za ugonjwa huo wa kuambukiza wa Ebola ni pamoja na homa kali, kudhoofika, maumivu ya misuli, kuumwa kichwa, koo kuwasha, kutapika, kuhara, kutokwa vipele na matatizo ya figo na ini.