Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni muhimu tusisahau yaliofanyika utumwani ili yasishuhudiwe tena:Ban

Ni muhimu tusisahau yaliofanyika utumwani ili yasishuhudiwe tena:Ban

Leo Machi 25 ni siku ya Kimataifa ya maadhimisho ya siku ya utumwa na biashara ya utumwa. Siku hii huadhimishwa kila mwaka na imetengwa kwa ajili ya kutoa fursa ya kuwaenzi na kuwakumbuka watu walioteseka na kufa mikononi mwa mfumo kandamizi wa utumwa. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Ushindi dhidi ya utumwa:Haiti na kwingineko.

Pia siku hii imetengwa kwa ajili ya kuhamasisha kuhusu hatari ya ubaguzi katika karne ya sasa.

Umoja wa Mataifa ulianza maadhimisho ya mwaka huu kwa onyesho la filamu Miaka 12 utumwani. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon aliyehudhuria onyesho hilo katika hotuba yake alisema kwamba alifahamu kupitia historia kwamba watumwa wengi maisha yao yalikuwa ni dhalili lakini hakuwa na mawazo kuwa yalikuwa ya kikatili namna hiyo.

(SAUTI YA BAN)

"Sikuweza kuamini! Najisikia vibaya sana vile ambavyo tunasimama na kufurahia manufaa yote tuliyo nayo hivi sasa duniani! Ni kwa vipi hatukuweza kuchukua hatua mapema zaidi kuokoa watu wote hao kutoka kwenye lindi la utumwa."

Katika ujumbe wake kwa mwaka huu Ban ameongeza kuwa ili kuwaenzi daima waathirika mnara wa kumbukumbu wa kudumu utajengwa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York.

Amesema mnara huo unatarajiwa kuwahamasisha watu katika juhudi za kuendelea kukabilina na mifumo tofauti ya utumwa unaoshuhudiwa zama za sasa.