Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchafuzi wa hewa wasababisha vifo vya watu Milioni Saba duniani kote: WHO

Uchafuzi wa hewa wasababisha vifo vya watu Milioni Saba duniani kote: WHO

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limetoa makadirio mapya ya vifo vya binadamu vitokanavyo na uchafuzi wa hali ya hewa ambapo mwaka 2012 pekee watu Milioni Saba walifariki dunia.

WHO inasema ripoti hiyo mpya inaweka bayana kuwa uchafuzi wa hewa ni moja ya athari kubwa zaidi ya afya itokanayo na uchafuzi wa mazingira na kwamba kupunguza uchafuzi wa mazingira kunaweza kuokoa uhai kwa mamilioni ya watu.

Kanda za Asia Mashariki na Kusini pamoja na Pasifiki Magharibi zimetajwa kuwa na kiwango kikubwa zaidi cha uchafuzi wa hewa ndani ya makazi na hata nje ya makazi na tatizo hilo ni kwa nchi tajiri na hata maskini.

WHO inasema takwimu hizo mpya zitokanazo na ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa kwa mwaka 2012, zinaonyesha uhusiano mkubwa zaidi wa kati ya uchafuzi wa hali ya hewa iwe ndani au nje na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile moyo na saratani.

Maria Neira ni Mkurugenzi wa Idara ya WHO inayohusika na afya ya umma.

(Sauti ya Maria)

“Kwa hiyo tunadhani hili ni jambo muhimu linalopaswa kuzingatia wakati tunachukua hatua za kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza na jinsi tunavyokabiliana na changamoto hizi zilizo mbele yetu.”

WHO inasema takwimu hizo mpya ni hatua muhimu kwa kuweka msingi wa kuzuia magonjwa yatokanayo na uchafuzi wa hewa.