Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuzingatia mchango wa Mandela kutasaidia kutokomeza ubaguzi

Kuzingatia mchango wa Mandela kutasaidia kutokomeza ubaguzi

Katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya kupinga ubaguzi, Umoja wa Mataifa unatoa wito kwa watu wote duniani hususan viongozi wa kisiasa, kidini na watetezi wa haki za kiraia kuimarisha mchango wa Hayati Mzee Nelson Mandela za kupiga vita ubaguzi wa rangi na chuki.

Katika ujumbe wake katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema hii ni mara ya kwanza siku hii inaadhimishwa bila ya Hayati Mandela na ni jambo linalotia machungu lakini pia inakumbusha ushindi wake uliovutia wengi dhidi ya sera za kibaguzi zilizomtia gerezani kwa miaka 27.

Amesema safari ya Mandela kutoka gerezani hadi kuwa Rais ni ushindi wa mtu wa kipekee dhidi ya nguvu za chuki, ujinga na woga na ni ushahidi wa uthabiti wa ujasiri, maridhiano na msamaha katika kukabiliana na ukosefu wa haki na ubaguzi wa rangi.

Katibu Mkuu ametaka siku hii itumike kutambua kuwa ubaguzi wa rangi umebakia kuwa tishio hatari na ni vyema kuchukua hatua ya kupatia suluhu kwa mashauriano na maridhiano yaliyodhihirishwa na waliotangulia. Amesema ni vyema kuheshimu na kutambua utofauti baina ya jamii kama utajiri .

Naye Mkurugenzi Mkuu wa shirika la elimu, sayansi na utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO, Irina Bokova amesema kutokuvumiliana kunadhoofisha dunia. Amesema dunia yapaswa kuongozwa na usawa bila kujali mazingira yoyote.