Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Moscow na Kiev waanze mazungumzo wazi : Ban

Moscow na Kiev waanze mazungumzo wazi : Ban

Mvutano unaoongezeka katika Ukraine na Urusi ni hatari kwa amani ya nchi hizo mbili na bara nzima, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon baada ya mkutano wake na raisi wa Urusi, Vladimir Putin.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Moscow, Bwana Ban amesisitiza umuhimu kwa pande zote mbili kuacha vitendo vya uchochezi, akiongeza kwamba kwenye historia vitendo vidogo vinaweza kusababisha baadaye hali isiyoweza kudhibitiwa.

Anasema alimweleza Rais Putin kwamba anaelewa wasiwasi wake kuhusu haki za watu wenye asili ya kirusi walio wachache nchini Ukraine, akirejelea umuhimu wa kuzingatia haki zao za kibinadamu na za watu wote nchini humo.

(Sauti ya Ban)

“Ni wazi kwamba tuko njiapanda. Inabidii tutumie njia zote za kidiplomasia ili tutatue huo mzozo, ambao una athari za kisiasa na kiuchumi. Dunia inatutizama na historia itatuhukumu jinsi tulivyowajibika kwa mujibu wa misingi ya mkataba wa umoja wa mataifa. Nitafanya vyovyote iwezekanavyo kusaidia kurejesha mawasiliano mazuri kati ya Urusi na Ukraine, nchi ambazo ni ndugu na ni wanzilishi wa Umoja wa mataifa. “

Katibu Mkuu ameomba pande zote kukaribisha wachunguzi wa haki za kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, walioanza kupelekwa sehemu mbali mbali za Ukraine.