Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yaonya ukosefu wa chakula na magonjwa CAR

WFP yaonya ukosefu wa chakula na magonjwa CAR

Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, Ertharin Cousin, ameonya kuhusu hali ya kutisha ya ukosefu wa chakula na utapiamlo, huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, kutokana na ghasia zinazoendelea na ukosefu wa fedha.

Akiwa ziarani nchini humo Bi Cousin, amesisitiza umuhimu wa kuchukua hatua hatua kabla msimu wa mvua haujaanza, ili wananchi waweze kupanda mazao yao akisema ikiwa wananchi wataendelea kukosa chakula, wanaweza kutumia mbegu zilizohifadhiwa kwa ajili ya kilimo. Amesema  mvua zinaleta changamoto kubwa katika usafirishaji wa chakula, na kusababisha magonjwa mbali mbali kama kuharisha.Elisabeth Byrs ni msemaji wa PAM, Geneva.

(Sauti ya Elizabeth Byrs) 

Tukishindwa kuwezesha familia kupanda mazao kabla ya msimu wa mvua, hakutakuwa na mavuno, kwa sababu ya ghasia, ukosefu wa usalama, swala kwamba watu wamekimbia makazi yao. Tunaona kwamba ukosefu wa uhakika wa chakula utaongezeka tena, na ni janga la kibinadamu ambalo liko mbele yetu, ikiwa hatutachukua hatua sasa hivi. 

Kuzorota kwa usalama  nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kulisababisha WFP kupeleka misaada yake kwa njia ya ndege ingawa sasa usafiri wa barabara unatumika lakini hali ya usalama haijaimarika vya kutosha.

Mzozo wa CAR umeshasababisha watu zaidi ya 290,000 kukimbia makazi yao na kuatafuta hifadhi nchi jirani hatua ambayo  pia inatishia amani katika nchi hizo.