Hali Jamhuri ya Afrika ya Kati ni mbovu mno: Pillay

20 Machi 2014

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, amesema hali mbovu mno. Bi Pillay amesema hayo wakati akihitimisha ziara yake ya siku mbili nchini humo, ambako amefanya mikutano na rais wa mpito, Waziri Mkuu, Waziri wa Sheria, mashirika ya umma, mashirika ya kibinadamu pamoja na makamanda wa vikosi vya kulinda amani. Joshua Mmali ana taarifa kamili

TAARIFA YA JOSHUA

Bi Pillay amewaambia waandishi wa habari kuwa ingawa mauaji kwa wingi kama yaliyofanyika mnamo na Disemba na Januari yamesitishwa kwa sasa kwa sababu ya kuwepo vikosi vya MISCA na Sangari, watu wanaendelea kuuawa kila siku, hususan na makundi yanayopinga Balaka.

Amesema Waislamu wapatao 15,000 wanaripotiwa kunaswa mjini Bangui na maeneo mengine kaskazini, kaskazini magharibi na kusini mwa nchi, wakiwa wanalindwa na vikosi vya kimataifa, lakini bado wanakabiliwa na hatari kubwa na hali isokubalika.

Bi Pillay ameongeza kuwa chuki baina ya jamii mbalimbali bado imetanda katika viwango vya kutisha, hasa ukizingatia aina ya mauaji yanayotekelezwa. Amesema nchini humo watu, siyo tu wanauawa, lakini wanateswa, kukatwakatwa, kuchomwa, wakati mwingine na makundi yanayoibuka ghafla, au makundi ya kupanga na yalojihami. Pillay ameongeza kuwa, ingawa CAR imeangaziwa na jamii ya kimataifa, haijaangaziwa kulingana na mahitaji yake.