Kifua Kikuu sugu chaendelea kuleta mkwamo: Mradi mpya kuleta matumaini: WHO

20 Machi 2014

Kifua Kikuu sugu kimeendelea kuwa changamoto kubwa kwa tiba dhidi ya ugonjwa huo limesema shirika la afya duniani, WHO wakati huu wa kuelekea siku ya kifua kikuu duniani hapo Jumatatu. WHO inasema mwaka 2012 pekee watu Laki Tano walikumbwa na ugonjwa huo na ni mtu mmoja tu kati ya wanne ambaye aliweza kuchunguzwa kutokana na uhaba wa huduma stahili. Alice Kariuki na ripoti kamili.

(Taarifa ya Alice)

Huku maudhui ya mwaka huu kwa siku ya kifua Kikuu ikiwa kufikia watu Milioni Tatu wanaotaka huduma ya uchunguzi na tiba dhidi ya ugonjwa huo, WHO inaamini kuwa mradi mpya wa kupanua wigo wa huduma utakuwa suluhisho katika nchi 27 unakotekelezwa. Mathalani inasema mradi huo uitwao EXPAND-TB utaongeza mara tatu idadi ya watu wanaofikiwa na huduma ya uchunguzi wakati huu ambapo ni theluthi Moja tu ya wagonjwa ndio wana uhakika wa uchunguzi.

Miongoni mwa nchi ambako mradi huo unatekelezwa ni Tanzania ambapo Naibu Meneja Mradi wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma Dokta Liberate Mleoh ameiambia Idhaa hii kuwa umekuja wakati muafaka na ni mkombozi.

(Sauti ya Dokta Mleoh)

WHO inasisitiza kuwa uchunguzi na tiba ya mapema dhidi ya aina zote za Kifua Kikuu ndio suluhisho la kupunguza idadi ya visa vya ugonjwa huo na hatimaye kuutokomeza.

Kwa mujibu wa WHO tangu mwaka 2009 hadi 2013 kulikuwa na visa

72,000 vya Kifua Kikuu sugu huku wagonjwa 36,000 wakibainika mwaka 2013 pekee.