Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo wa Ukraine-Urusi unabadilika kutoka kisiasa kuwa wa kijeshi: Eliasson

Mzozo wa Ukraine-Urusi unabadilika kutoka kisiasa kuwa wa kijeshi: Eliasson

Wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akielekea Urusi na Ukraine kwa ajili ya kusaka suluhu la kidiplomasia kwenye mzozo wa pande mbili hizo juu ya Crimea, baraza la usalama limeelezwa kuwa mambo yanayojitokeza kila uchwao kwenye eneo hilo yanaweza kuzorotesha amani zaidi huku hali ya haki za binadamu Ukraine na Crimea ikielezwa kuwa ni ya kutia shaka.

Katika kikao cha leo, Naibu Katibu Mkuu Jan Eliasson ambaye alikwenda Ukraine, amewaeleza wajumbe kuwa dalili zinaonyesha kuwa mzozo huo sasa unabadilika kutoka kuwa wa kisiasa na kuwa wa kijeshi.

Amesema hayo akizingatia ripoti za hivi karibuni kuhusu kuuawa kwa afisa wa kijeshi wa Ukraine mbele ya kituo cha kijeshi kwenye viunga vya mji wa Simferopol na Rais wa Urusi kutambua Crimea kuwa ni eneo huru kutoka Ukraine.

Amesema mvutano kati ya Ukraine na Urusi unahatarisha usalama na amani duniani na ni lazima diplomasia itumike kwa kuzingatia kuwa nchi hizo ni majirani.

(Sauti ya Eliasson)

Ivan Šimonovic Naibu msaidizi wa katibu Mkuu kuhusu haki za binadamu baada ya kurejea kutoka maeneo hayo alisema hali ya haki za binadamu ni ya kutia shaka, akigusia hali ya Ukraine na huko Crimea ambako mwili wa mtetezi wa haki za binadamu ulipatikana umetelekezwa.

(Sauti ya Ivan)