Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dokta Kelemu miongoni mwa washindi wa tuzo ya UNESCO na L’Oreal

Dokta Kelemu miongoni mwa washindi wa tuzo ya UNESCO na L’Oreal

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO kwa kushirikiana na taasisi ya L’Oreal leo wanaendelea na utaratibu wao wa kila mwaka wa kuwapatia tuzo wanawake watano wanasayansi kila mwaka kutokana na mchango wao utafiti kwenye jamii zao.

Wanawake hao, mmoja kutoka kila bara wanawakilisha mwelekeo wa kipekee wa kitaalamu ndani ya nyanja ya sayansi uliojumuishwa na kipaji cha kipekee na kujitoa kwa dhati kijasiri kwenye fani hiyo iliyotawaliwa zaidi na wanaume.

Miongoni mwao ni Dokta Segenet Kelemu kutoka Ethiopia ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi Mkuu wa kituo cha utafiti wa wadudu na Ikolojia huko Nairobi, Kenya akiwakilisha bara la Afrika na nchi za kiarabu.

Akiwa ni mwanamke wa kwanza kusoma katika chuo kikuu cha mwanzo kabisa nchini mwake Ethiopia, Dokta Kelemu anapatiwa tuzo kutokana na utafiti aliofanya juu ya vijidudu na uwezo wao wa kukabiliana na magonjwa na mabadiliko ya tabianchi.

Washindi wengine wa tuzo hiyo iliyoanza kutolewa mwaka 1998 ni Profesa Brigite Kieffer akiwakilisha Ulaya, Profesa Laurie Glimcher , Amerika Kaskazini, Profesa Cecilia Bouzat Amerika Kusini na Profesa Kayo Inaba Asia na Pasifiki.