Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujenzi wa amani baada ya migogoro waangaziwa katika Baraza la Usalama

Ujenzi wa amani baada ya migogoro waangaziwa katika Baraza la Usalama

Milipuko ya machafuko ya hivi karibuni katika Sudan Kusini na Jamhuri ya afrika ya Kati ni ishara dhahiri ya mazingira yasotabirika katika ujenzi wa amani, na hatari zinazohusika na harakati hizo. Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson katika hotuba yake kwa Baraza la Usalama, ambalo limekutana kujadili suala la ujenzi wa amani baada ya migogoro. Priscilla Lecomte ana taarifa kamili

(TAARIFA YA PRISCILLA)

Katika hotuba yake, Bwana Eliasson amesema ni vyema kujiandaa na kutafuta mbinu mpya za kujenga amani, kutokana na uzoefu na ushahidi yakinifu. Amerejelea ujumbe wa Katibu Mkuu, ambao ulitambua mambo matatu muhimu ambayo yanapaswa kuangaziwa katika ujenzi wa amani.

Ameyataja mambo hayo kama ujumuishaji, ujenzi wa taasisi na usaidizi endelevu wa kimataifa na uwajibikaji.

Mikataba ya amani ambayo huwajumuisha tu watu wachache,mara nyingi hushindwa kutimiza matakwa na matarajio ya watu, na hivyo huwa hafifu. Ingawa mikataba ya amani inatakiwa kuwajumuisha watu wenye silaha, ujenzi wa amani kimsingi unahitaji harakati za kisiasa ambazo zinajumuisha watu wote na uwajibikaji wa umma.”

Awali, Baraza hilo la Usalama kwa kauli moja limepitisha azimio la kulaani uuzaji haramu wa mafuta ya Libya, na kuitaka serikali ya Libya kutoa habari kwa haraka kuhusu bendera za nchi ambazo meli zake zinahusika katika uuzaji huo, na serikali za nchi hizo kuwajibika katika kuhakikisha kuwa meli hizo haziingizi mafuta hayo haramu katika maeneo ya mipaka yake.