Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mgao wa chakula wasambazwa kwa anga huko Sudan Kusini: WFP

Mgao wa chakula wasambazwa kwa anga huko Sudan Kusini: WFP

Nchini Sudan Kusini , Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limeanza kazi ya kusambaza kwa njia ya anga msaada wa dharura wa chakula kwenye maeneo ya ndani zaidi ambayo ni magumu kufikika kutokana sababu mbali mbali ikiwemo ukosefu wa usalama.

Operesheni hiyo imeanza kwa ajili ya kulisha waathirika wa mzozo unaoendelea na kwenye kambi ambazo mgao wa awali umemalizika.

Mwakilishi mkazi wa WFP nchini Sudan Kusini Chris Nikoi amesema wanahaha kufikisha msaada kwa wahitaji kwa njia hiyo ya anga kwa kuwa wameshindwa kufikia sehemu hizo kwa barabara au boti.

Mgao wa jumanne kwa njia ya anga umefikia wakimbizi wa ndani Elfu Nane kwenye mji wa Ganyiel jimbo la Unity na unatarajiwa kuwatosheleza kwa siku 15.

Maeneo mengine Tisa yatakayonufaika na mgao kwa njia ya anga yapo kwenye majimbo ya Upper Nile, Jonglei na Unity states na kuna mpango wa kujumuisha maeneo mengine.