Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM walaani vikali shambulio la kujilipua huko Afghanistan

UM walaani vikali shambulio la kujilipua huko Afghanistan

Umoja wa Mataifa umelaani vikali shambulio la kujilipua lililotokea Jumanne huko jimbo la Faryab, Kaskazini mwa Afghanistan na kusababisha vifo vya raia 15 na wengine wapatao 50 wamejeruhiwa.

Ripoti zinasema mshambuliaji akiwe amejifunga mwilini vilipukaji alijilipua katikati mwa mji mkuu wa jimbo hilo, Maimana ambapo kituo cha afya kimeripoti kuwa miongoni mwa waliouawa ni watoto wawili na mwanamke mjamzito ni miongoni mwa majeruhi.

Naibu Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan Nicholas Haysom amesema ongezeko la vifo vya raia kutokana na vilipukaji ni janga na kwamba matumizi yake kwenye maeneo kama vile masoko hayakubaliki.

Amesisitiza wito wa mara kwa mara kutoka ofisi ya umoja wa mataifa nchini humo UNAMA ya kusitisha mara moja matumizi ya vilipukaji hivyo hususan kwenye maeneo yenye raia wengi.

Tangu kuanza kwa mwaka huu raia zaidi ya 190 wameuawa kutokana na mashambulio yanayotumia vilipukaji hivyo kiwango ambacho ni ongezeko kwa asilimia 14 ikilinganishwa na mwaka jana.

Shambulio la leo limekuja wakati Afghanistani inajiandaa kwa uchaguzi wa Rais na majimbo tarehe Tano mwezi ujao.