Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtaalamu wa UM kuhusu Mynmar awasilisha ripoti yake ya mwisho

Mtaalamu wa UM kuhusu Mynmar awasilisha ripoti yake ya mwisho

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Mynmar Tomás Ojea Quintana,leo amewasilisha rasmi ripoti yake ya mwisho inayoelezea hali jumla ya haki za binadamu katika kipindi cha miaka 6 kabla ya kumaliza muhula wake baadaye mwaka huu.

Mtaalamu huyo ambaye amewasilisha ripoti hiyo mbele ya baraza la haki za binadamu imezitaja hatua zilizopigwa na taifa hilo ikiwemo kuboreshwa kwa mifumo inayozingatia haki za binadamu.

Amesema kuwa pamoja na taifa hilo kuandamwa na matatizo mbalimbali ikiwemo mapigano ya ndani yaliyodumu kwa muda mrefu, hatimaye mwanga mpya wa matumaini umeanza kuchomoza na hivyo kutoa ishara kwamba taifa hilo lipo katika mwelekeo sahihi.

Amepongeza pia mageuzi yanayoendelea kutekelezwa nchini humo ikiwemo yale yanayohusu maeneo ya uhuru wa habari na nafasi ya mashirika ya kiraia.

Mtaalamu huyo anatazamiwa kumaliza kipindi chake baadaye mwezi huu, na baraza hilo la haki za binadamu linatazamiwa kujaza nafasi hiyo kwa kumchagua mjumbe mwingine.