Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pillay kuizuru Jamhuri ya Afrika ya Kati

Pillay kuizuru Jamhuri ya Afrika ya Kati

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, atafanya ziara ya siku tatu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, ili kuzungumzia hali mbaya ya haki za binadamu nchini humo na serikali ya mpito, taasisi muhimu za kimataifa na vikosi vya kulinda usalama. Alice Kariuki na taarifa kamili

(TAARIFA YA ALICE)

Katika ziara yake, Bi Pillay amepanga kukutana na kiongozi wa serikali ya mpito, Catherine Samba-Panza, Waziri Mkuu pamoja na mawaziri wa sheria, maridhiano na mawasiliano. Atakutana pia na wawakilishi wa Muungano wa Afrika, AU, Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika ya Kati, pamoja na mabalozi wa EU na Ufaransa.

Akiwa mjini Bangui, Kamishna huyo mkuu atakutana pia na mwakilishi wa rais wa Kamisheni ya AU na mkuu wa vikosi vya kulinda amani vya AU, MISCA, pamoja na wawakilishi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyomo nchini humo.

Amepanga pia kuzuru maeneo ya uharibifu na kukutana na baadhi ya watu wapatao 650,000 ambao wamelazimika kuhama makwao CAR. Mwishoni mwa ziara yake mnamo Alhamis, Bi Pillay atakutana na waandishi wa habari.