Baraza la Usalama laongeza muda wa UNSMIL Libya

14 Machi 2014

 

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limepitisha azimio la kuongeza muda wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuisaidia Libya, UNSMIL hadi tarehe 13 Machi  2015. Kwa mujibu wa azimio hilo, UNSMIL itaendelea kusaidia katika juhudi za serikali ya mpito za kukaribisha democracia, ikiwemo kupitia kuendeleza na kutoa ushauri wa kitaalam na mazungumzo ya kitaifa.

Ujumbe huo pia utahitajika kuendeleza utawala wa sheria na kuangalia na kulinda haki za binadamu, hususan zile za akina mama na watoto, kulingana na majukumu ya Libya chini ya sheria ya kimataifa. UNSMIL itahitajika pia kudhibiti silaha na kupambana na uzagaaji wa silaha hizo, pamoja na kujenga uwezo wa Libya kujitawala.

Katika muktadha huo, azimio hilo la Baraza la Usalama linaitaka serikali ya Libya kuboresha udhibiti wake wa silaha na vifaa vinginevyo vya vita, na kuangalia jinsi vinavyoagizwa au kuuzwa Libya, pamoja na kulaani ukiukwaji wa maazimio ya awali kuhusu udhibiti wa silaha.

Baraza la Usalama pia limeazimia kuunga mkono juhudi za kuokoa fedha zilizoporwa chini ya serikali ya Muammar Qadhafi, na kuziomba nchi ambazo zimeziweka fedha na mali hizo kushauriana kuhusu madai ya uporaji wa mali hizo.