Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kinachoendelea Burundi chamtia hofu Katibu Mkuu wa UM

Kinachoendelea Burundi chamtia hofu Katibu Mkuu wa UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema anasikitishwa sana na kile kinachoendelea hivi sasa nchini Burundi hususan ghasia na vurugu za wiki iliyopita kati ya polisi na wafuasi wa vyama vya upinzani nchini humo.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imemkariri Katibu Mkuu akisema kuwa serikali na vyama vya siasa ni lazima wajizuie na wajiepushe na vitendo vyovyote ambavyo vinaweza kuchochea ghasia zaidi.

Hata hivyo ameshutumu kuendelea kubinywa kwa uhuru wa kujieleza, mkusanyiko hususan kuzuiwa au kuharibiwa kwa mikutano ya vyama vya upinzani vya kisiasa kunakofanywa na polisi na vijana wa chama tawala.

Bwana Ban amesema kuheshimu uhuru huo na haki nyingine za haki za binadamu ni moja ya vigezo vya kuhakikisha uchaguzi wa mwaka 2015 unakuwa huru na salama. Amesema Burundi haipaswi kupoteza fursa hiyo na ameisihi serikali, viongozi wa kisiasa na wawakilishi wa vikundi vya kiraia kushirikiana ili kuepusha kuzidi kuzorota kwa usalama.

Amesema Umoja wa Mataifa kwa upande wake uko tayari kuendelea kutoa usaidizi kwa lengo hilo.

Amerejelea wito wake wa kutoka serikali na vyama vya siasa kuzindua kampeni dhidi ya ghasia za kisiasa wakati huu wa kueleka uchaguzi mkuu na kupatia suluhu ya mizozo kati yao kwa njia ya amani na mashauriano kwa kuzingatia makubaliano yaliyoridhiwa mwezi Machi mwaka jana kwa mujibu wa mikataba ya Arusha.