Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan Kusini mapigano, mafuriko vyakwamisha usaidizi: DRC-Kivu Kaskazini hali yazidi kuimarika: UM

Sudan Kusini mapigano, mafuriko vyakwamisha usaidizi: DRC-Kivu Kaskazini hali yazidi kuimarika: UM

Mapigano yanayoendelea kwenye majimbo ya Jonglei, Upper Nile na Unity huko Sudan Kusini yanasababisha watu kukimbia makazi yao na kukwamisha jitihada za kuwafikishia misaada ya dharura, imesema ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu misaada ya kibinadamu, OCHA.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephen Dujarric amewaambia waandishi wa habari kuwa hivi sasa watoa misaada wanahaha kupata kibali cha pande zote kwenye mapigano hayo ili kupata mahitaji ya kibinadamu yaliyoporwa pamoja na kuwezesha operesheni za usaidizi kufikia wahitaji kwa usalama

Halikadhalika huko Juba, mvua kubwa zilizonyesha eneo hilo linakwamisha juhudi za usaidizi kwa wakimbizi kwenye kambi ya ofisi ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS na kwamba kuanzia jana wameanza kuhamishia wakimbizi hao maeneo mengine.

Huko DRC, inaelezwa kuwa kurejea kwa amani kwenye vijiji kadhaa vya jimbo la Kivu Kaskazini kumesababisha wananchi kurejea makwao. Hapo jana mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa huko Goma aliweka bayana kuwa vikundi vilivyojihami kamwe visikubaliwe madai yao kuwa vinawakilisha jamii au kabila Fulani na badala yake vijisalimishe mapema iwezekanavyo