Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi za Asia na Pasifiki zaombwa kushiriki mchakato wa kutokomeza njaa

Nchi za Asia na Pasifiki zaombwa kushiriki mchakato wa kutokomeza njaa

Juhudi za kutokomeza njaa katika ukanda wenye watu wengi zaidi duniani zimepigwa jeki kufuatia baadhi ya nchi kuitikia vyema wito wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo, FAO wa kuongeza juhudi za kutomomeza njaa katika maeneo ya Asia na Pasifiki.

Akizungumza wakati wa kongamano la FAO la 32 katika ukanda huo, Mkurugenzi Mkuu wa FAO Jose Graziano da Silva amepongeza matokeo ya kufurahisha yaloonekana katika baadhi ya nchi za ukanda huo katika kupunguza njaa.

Bwana da Silva amesema Thailand na Viet Nam zimepunguza idadi ya watu wasio na chakula kwa asilimia 80, huku China ikifikia lengo la milenia la kupunguza idadi ya watu wenye njaa kwa nusu ifikapo mwaka 2015. Ameongeza kuwa katika bara Asia kwa ujumla, kiwango cha njaa kimepungua kutoka asilimia 24 kati ya mwaka 1990 na 1992, hadi asilimia 13.5 kati ya mwaka ya 2011 na 13.

Amesema huku ukanda huo ukiwa kwenye mkondo sahihi wa kufikia lengo la milenia la kupunguza njaa, juhudi zaidi zinatakiwa kufanywa, kwani hata kiwango kikifikia asilimia 12 inayolengwa, bado ukanda huo utakuwa na watu milioni 500 wenye njaa, ukizizidi kanda nyingine zote duniani.