Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ongezeko la vyakula vilivyokuzwa kijenetiki lakwamisha biashara baina ya nchi: FAO

Ongezeko la vyakula vilivyokuzwa kijenetiki lakwamisha biashara baina ya nchi: FAO

Shirika la Chakula na Kilimo duniani, FAO limesema bidhaa za mazao zinazouzwa baina ya nchi zimebainika kuwa na kiwango kidogo cha mazao yanayokuzwa kwa kutumia marekebisho ya kijenetiki, GMO na hivyo kusababisha bidhaa hizo kurejeshwa zilikotoka au kuteketezwa.

FAO inasema uchanganyaji huo huenda hufanyika bahati mbaya wakati wa uzalishaji, upakiaji, uhifadhi au usafirishaji wakati huu ambapo kuna ongezeko la uzalishaji wa bidhaa hizo duniani.

Sarah Cahill ni afisa wa usalama wa chakula FAO anasema hofu ni biashara kuporomoka baina ya nchi na gharama za kuteketeza lakini kuna usalama wa walaji..

(Sauti ya Sarah)

Tunafahamu walaji wengi wanapenda kuchagua kati ya vyakula vya GMO na visivyo vya GMO kwa hiyo kama haiko bayana kuwa ni GMO kamili au ina kiwango kidogo cha GMO, hilo litaathiri chaguzi lao! Wanaweza wasiwe na taarifa za kutosha za kuwezesha kufanya uamuzi wao.”

Shirika hilo limesema kwa sasa kuna ongezeko la uzalishaji wa GMO duniani na kwamba kutokuwepo kwa mkataba wa kimataifa kuhusu kiwango cha GMO kinachokubalika kwenye mazao ya kawaida, kunafanya kila nchi kuwa na ainisho lake.

FAO inasema nchi 26 zilizuia baadhi ya mazao baada ya kubaini uwepo kiwango cha GMO na mazao husika zaidi ni pamoja na mchele, mapapai na mahindi.