Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali zilinde uhuru wa kuabudu ili kukabiliana na chuki za kidini: UM

Serikali zilinde uhuru wa kuabudu ili kukabiliana na chuki za kidini: UM

Mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya kuwa na imani au dini, Heiner Bielefeldt, ametoa wito kwa serikali ziendeleze na kuulinda uhuru wa kila mmoja kuwa na dini au imani, ili kukabiliana na tatizo linalozidi kukua la chuki za kidini duniani.

Bwana Bielefeldt, ambaye amekuwa akiwasilisha ripoti yake mpya kwa Baraza la Haki za Binadamu mjini Geneva, amesema vitu vinavyodhihirisha chuki za halaiki huwa havilipuki kama volcano, lakini huwa vinaanzishwa na wanadamu, ambao vitendo vyao vinaweza kuchangia hali mbovu katika jamii, mithili ya majanga ya kiasili.

Ameonya kuwa hisia za chuki ya halaiki aghalabu husababishwa na mjumliko wa hofu na madharau, ambavyo vinaweza kuibua kutoaminiana, misimamo mikali na msisimko wa halaiki. Ametoa wito kwa serikali zijikite katika kujenga kuaminiana kupitia taasisi za umma, ili kuwahakikishia watu kuwa wana uhuru wa kuabudu au kuwa na imani yoyote.

Ripoti hiyo inaorodhesha baadhi ya vitu vinavyochangia kudhihirika lwa chuki za kidini, kama vile ufisadi ulokithiri na utawala wa kiimla ambao hubana mazingira yanayoruhusu uhuru wa watu kujieleza hadharani katika mijadala, na hivyo kuweka dhana za kushuku.