Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali huko Ukraine yazidi kumtia wasiwasi Katibu Mkuu

Hali huko Ukraine yazidi kumtia wasiwasi Katibu Mkuu

Naendelea kutiwa hofu na kile kinachoendelea huko Ukraine kwani tangu kuanza kwa mzozo huo nimesihi pande zote kupunguza mvutano na kushiriki kwenye mashauriano lakini bado hali inasikitisha!

Ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon aliyoitoa kupitia msemaji wake Stéphane Dujarric hii leo. Amesema kuwa matukio ya hivi karibuni huko Crimea yamezidi kutwamisha mzozo huo na kadri mvutano na kutokuaminiana kunavyozidi kuongezeka, yeye anazisihi pande zote kujiepusha na vitendo na kauli za kichochezi.

Katibu Mkuu ametaka jumuiya ya kimataifa kusaidia wahusika wakuu wa mzozo huo katika kupunguza mvutano na kuelekea mchakato wa kupatia suluhu la kisiasa huku wakiheshimu utaifa, uhuru na mamlaka ya Ukraine.

(Sauti ya Dujarric)

“Mvutano na kutokuamiana kunazidi kuongezeka na hivyo anazisihi pande zote kujizuia kuchukua hatua za haraka na kurushiana kauli za kichochezi. Na zaidi ya yote suluhu la mzozo huo linapaswa kuzingatia misingi ya katiba ya Umoja wa Mataifa ambayo ni kutatua mizozo kwa amani.”

Wakati huo huo imeelezwa kuwa Baraza la Usalama baada ye leo litakuwa na kikao cha faragha kuhusu Ukraine.