Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa CSW58 waanza leo, Maziwa Makuu na Ukanda wa Sahel wamulikwa:UNFPA

Mkutano wa CSW58 waanza leo, Maziwa Makuu na Ukanda wa Sahel wamulikwa:UNFPA

Mkutano wa 58 wa Kamisheni kuhusu hali ya wanawake duniani, CSW58 unaanza leo mjini New York, Marekani ambapo moja ya vikao vya ngazi ya juu vitavyofanyika ni kuhusu mwelekeo wa jamii kwenye ukanda wa Sahel na ukatili wa kijinsia kwenye nchi za maziwa makuu barani Afrika.

Akizungumzia katika mahojiano maalum na Yasmin Guerda wa kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu UNFPA Dkt. Babatunde Osotimehin amesema kikao hicho ni cha kwanza kufanyika na kinafuatia ziara katika maeneo hayo zilizofanywa mwaka jana na viongozi waandamizi wa Umoja wa Mataifa akiwemo Katibu Mkuu Ban Ki-Moon na Rais wa Benki ya dunia kwenye maeneo hayo na kubaini umuhimu wa kuonisha harakati za amani na usalama na zile za maendeleo hasa kwa kujenga ushirikiano baina ya nchi husika.

Ametolea mfano eneo la maziwa makuu hususan Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Cono, ambapo walibaini migogoro kuwa kichocheo cha ukatili wa kijinsia na hata watoto wa kike kushindwa kwenda shule ilhali Ukanda wa Sahel mazingira ni magumu na jambo muhimu ni kujengea uwezo vijana ili waweze kujikwamua.

Tulibaini kuwa katika maeneo hayo ya Afrika, na hata duniani kote unapoleta stadi pamoja na kubadilishana uzoefu, na unakuwa na kikao cha ushirkiano wa nchi za Kusisni, huna sababu ya kubuni upya! Kuna mambo ambayo yanatokea nchi moja au nyingine na unaweza kuyachukua mara moja na kutumia nchi nyingine. Hilo ni moja, na pili, kwa kuzngatia mazingira ya kipekee kwenye ukanda wa Maziwa makuu, kushirikiana katika mambo ya aina hiyo inapunguza mvutano. Usalama wa binadamu linakuwa ni kipaumbele, hivyo mzozo unaoona utatoweka, biashara ya mipakatni itaimarika na utaona hakuna sababu ya kugombana, na naamini hiyo ni hatua nzuri sana kuchukua.”

Mkurugenzi Mtendji huyo wa UNFPA akazungumzia vile maeneo hayo mawili yanavyoshabihiana..

(Sauti ya Dkt. Osotimehin)

Katika maeneo hayo mawili, jambo moja ambalo naona yanashabihina ni suala la msichana barubaru ambaye haendi shule, hajawezeshwa, hana stadi na uwezo wa kutambua anatakua kuwa nani. Kwangu mimi kama kuna kundi ambalo ningetaka kulipatia uwezo ni hilo. Msichana huku pia anawasilisha wasichana wengine duniani, barani afrika na hata kusini mwa Asia ambako tunaona suala hilo linatia shaka sana. Tunaona pia baadhi ya sehemu za Ulaya, ambako watoto hawajitambui, hawana huduma za afya, hawajui watakuwa nani! Haki zao zinakiukwa wapo wanaokumbwa na ukeketaji. Nafikiri tunapaswa kufanya kazi zaidi, iwapo tutapatia suluhu mambo yanayokumba wasichana barubaru basi tunaweza kubadili dunia.”

Kikao hicho kimeandaliwa na UNFPA kwa ushirikiano na Benki ya dunia.