Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akaribisha uamuzi wa ICC dhidi ya Katanga

Ban akaribisha uamuzi wa ICC dhidi ya Katanga

Baada ya Mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC huko The Hague kutangaza kumpata na hatia German Katanga ya makosa matano ikiwemo uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amekaribisha hatua hiyo akisema ni muhimu kwa wahanga wa tukio la shambulio husika kwenye kijiji cha Bogoro, wilaya ya Ituri Mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo mwezi Februari mwaka 2003.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imemkariri Bwana Ban akisema kuwa hatua hiyo pia ni muhimu kwa haki ya kimataifa na kwa hatua za kuepuka ukwepaji wa sheria huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Amerejelea kujizatiti kwa Umoja wa Mataifa kuunga mkono kazi ya mahakama hiyo kama kitovu ya mfumo wa haki wa kimataifa.

Halikadhalika Katibu Mkuu amesifu kitendo cha ushirikiano unaoendelea kuonyeshwa na serikali ya DRC na ICC na kutaka mamlaka za nchi hiyo kuendelea kuimarisha jitihada zake za kuwajibisha wahusika wote wa vitendo vya uhalifu vinavyotia shaka jamii ya kimataifa.

ICC imetangaza kuwa hukumu na suala la fidia kwa wahanga wa tukio hilo vitatolewa baadaye.