Usawa wa wanawake haimaanishi wanaume wanapoteza nguvu: Mkuu UN-Women Tanzania

8 Machi 2014

Wakati Tanzania leo inaungana na dunia kuadhimisha siku ya wanawake duniani, Mkuu wa ofisi ya shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na wanawake UN-Women nchini Tanzania Anna Collins Falk amesema ujumbe wa mwaka huu umekuja wakati muafaka ili kuondoa dhana inayodhani kuwa lengo la usawa kwa wanawake ni kuengua wanaume.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Stella Vuzo wa Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa nchini humo, Bi. Falk amesema ujumbe huo unashughulikia shaka na shuku katika baadhi ya jamii…

(Sauti ya Anna Collins Falk)

“Kwa ukweli ni ujumbe thabiti sana ukiufikiria! Usawa kwa wanawake ni maendeleo kwa wote. Kwa sababu unashughulikia hofu.. kwamba kwamba haki za wanawake haimnaanishi wanaume wanapoteza uthabiti! Na wanawake wakiwezeshwa haimaanishi wanaume wanakuwa hawana uwezo au wanapoteza mamlaka zote. LA hasha! Ina maana kwamba kila mtu ananufaika, ina maana kwamba iwapo utawekeza katika kuwezesha wanawake na kuna usawa wa kijinsia, kuna uwezekano wa kila mtu kuibuka mshindi.”

Ametolea mfano wa Kilimo ambacho amesema ni sekta inayohusisha wanawake wengi Tanzania na hivyo wakienguliwa katika mafunzo, huduma za ughani, hiyo itaathiri kipato cha familia kutokana na nafasi yao muhimu katika utunzaji wa kaya.

Nchini Tanzania maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yatafanyika kimkoa ambapo jijini Dar es salaam yatafanyika wilaya ya Temeke.