Katanga apatikana na hatia huko ICC, hukumu kutolewa baadaye

7 Machi 2014

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu huko the Hague, ICC imemkuta na hatia ya makosa matano Germain Katanga ambaye alishtakiwa kwa makosa kumi ikiwemo uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita.

Uamuzi huo wa jopo la majaji umesomwa na Jaji Bruno Cotte akitaja makosa hayo kuwa ni moja dhidi ya uhalifu wa kibinadamu kwenye mauaji na Manne ya uhalifu wa kivita ikiwemo kushambulia raia na uharibifu wa mali.

Jaji Cotte amesema kupitia shuhuda za mashahidi na ushahidi uliowasilishwa mahakamani, wamethibitisha pasipo shaka kuwa mshtakiwa alichangia kwa kiasi kikubwa kwa vitendo vilivyotekelezwa na wanamgambo wa Ngiti huko Bogoro jimbo la Ituri Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, mwezi Februari mwaka 2003.

Mahakama imeona kuwa Katanga aliimarisha uwezo wa wanamgambo hao kushambulia na hivyo amepatikana na hatia ya mauaji na katika kosa moja dhidi ya uhalifu wa kibinadamu

Hata hivyo mahakama haikumpata na hatia kwenye makosa mengine ikiwemo ubakaji na utumikishaji wa watoto jeshini kwani imesema hakukuwepo na ushahidi wa kutosha kuthibitisha mashtaka hayo.

Hukumu dhidi ya Katanga na fidia kwa waathirika itatajwa baadaye huku mahakama ikisema kuwa upande wa mashtaka na utetezi una haki ya kukata rufaa uamuzi huo ndani ya siku 30 kuanzia leo.

Kesi dhidi ya Katanga ilianza tarehe 24 Novemba 2007.