Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali katika CAR yahitaji hatua za dharura: Valerie Amos

Hali katika CAR yahitaji hatua za dharura: Valerie Amos

Mkuu wa Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu na Masuala ya Dharura katika Umoja wa Mataifa, Valerie Amos, amesema kuwa hali katika Jamhuri ya Afrika tya Kati ni mbaya mno na hatua za dharura zinahitajika ili kuepusha umwagaji damu zaidi.

Bi Amos amesema hayo wakati akilihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na kuongeza kuwa machafuko nchini humo yamesababisha kuharibika kwa utawala mashinani na kitaifa, na taasisi za kitaifa ambazo zilikuwa dhoofu sasa zimesambaratika kabisa . Ameongeza kuwa serikali haina uwezo wa kutoa huduma za kimsingi, wala uwezo wa kukomesha wimbi la machafuko.

CAR inashuhudia ukatili wa kidini usokubalika, ukosefu wa usalama na kuenea kwa hofu. Zaidi ya watu 650,000 bado ni wakimbizi wa ndani kote nchini, na zaidi ya 232,000 mjini Bangui pekee. Watu 70,000 bado wanaishi kwenye kituo cha wakimbizi kwenye uwanja wa ndege katika mazingira yanayotisha, na ambayo yanatarajiwa kuzorota zaidi msimu wa mvua utakapoanza. Iwapo hali ya sasa haiwezi kubadilishwa, mkondo wa mabadiliko ya watu na kijamii utakuwa na madhara ya kudumu kwa taifa hilo, ukanda na bara zima”

Bi Amos ambaye aliizuru CAR hivi karibuni, amesema kuwa jamii ambazo zimeishi pamoja kwa miaka mingi sasa haziaminiani tena. Ameongeza kuwa watu katika ngazi zote walimwambia yeye na ujumbe wake kuwa, ingawa dini na ukabila unabainika katika mapigano, mzozo huo si wa kidini, bali dini inatumiwa na watu kwa ajili ya malengo yao ya kisiasa na kiuchumi.