Hatua zimepigwa katika kuteketeza silaha za kemikali Syria: Kaag

5 Machi 2014

Mkuu wa Ujumbe wa pamoja wa kuteketeza silaha za kemikali za Syria, Sigrid Kaag, amesema katika siku chache zilizopita, serikali ya Syria imeongeza kasi ya juhudi za kuteketeza silaha zake za kemikali, na kwamba kuna uwezekano wa kuhitimisha shughuli hiyo ifikapo tarehe ya mwisho ilowekwa ya Juni 30, 2014 ikiwa serikali hiyo itazingatia ratiba yake mpya ilofanyiwa marekebisho.

Baada ya kulihutubia Baraza la Usalama, Bi Kaag ambaye anaongoza ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa na Shirika la Kupinga Silaha za Kemikali, OPCW, amewaambia waandishi wa habari kuwa tayari shehena kadhaa zimesafirishwa, na nyingine zitaendelea ili kuondoa silaha hizo.

Amesema ukijumulisha uondoaji na uteketezaji, ujumbe huo tayari ama umeondoa au kuharibu angaa thuluthi moja ya silaha za kemikali na kemikali za sumu nchini Syria.

“Bila shaka takwimu hizi zitabadilika. Tunapoendelea katika siku chache zijazo, tunatarajia kufikia asilimia 40 hadi 41. Na juhudi zaidi zikiendelea kufanywa na kuungwa mkono na jamii ya kimataifa, tunatarajia kuona hatua zaidi. Lakini bado ni kazi ngumu, inayohitaji kujitoa sana na utashi wa kutekeleza. Tumehakikishiwa na mamlaka katika ngazi ya juu zaidi kuwa haya yataendelea”.

Bi Kaag amesema mwezi huu wa Machi, ni muhimu sana katika hatua za kufikia tarehe ya miwsho.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter