Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wafunga pazia la ofisi yake ya kisiasa Sierra Leone, UNIPSIL

UM wafunga pazia la ofisi yake ya kisiasa Sierra Leone, UNIPSIL

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon leo ameshuhudia kuhitimishwa kwa jukumu la ofisi ya Umoja huo ya kisiasa na ujenzi wa amani Sierra Leone, UNIPSIL na kuelezea shukrani zake kwa ushirikiano uliotolewa na wananchi na serikali wakati wa kipindi chote cha zaidi ya miaka 15 ya operesheni za ofisi hiyo na zilizotangulia. Taarifa zaidi na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Akizungumza mjini Freetown katika mkutano na waandishi wa habari uliohudhuriwa pia na Rais Ernest Bai Koroma, Bwana Ban hata hivyo amesema ofisi ya mwakilishi mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini humo itaendelea kama kawaida na itafanya kazi kwa karibu na serikali.

Bwana Ban amesema ni fahari kubwa kushuhudia mafanikio ya operesheni za Umoja huo nchini Sierra Leone kuanzia UNAMSIL hadi UNIPSIL na kwamba nchi hiyo sasa ni mfano wa kuigwa duniani katika mafanikio ya ulinzi na ujenzi wa amani pamoja na kuibuka baada ya mzozo.

Amesema kinachoshuhudiwa sasa ni harakati za maendeleo ya kudumu na amepongeza nchi hiyo kwa kuhitimisha michakato mitatu ya uchaguzi wa kidemokrasia tangu kumalizikwa kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Bwana Ban amesema baada ya kuhitimishwa kwa shughuli za UNIPSIL wanatambua umuhimu wa jitihada za kujenga nchi yenye amani na ustawi zaidi kwa kuzingatia misingi ya uongozi wa kisheria na utawala bora.