Ujumbe wa mwaka huu kwa siku ya wanawake ni dhahiri: Mkuu UN-Women

7 Machi 2014

Usawa kwa wanawake ni maendeleo kwa wote ni ujumbe wa siku ya wanawake duniani mwaka huu wa 2014 ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na wanawake Phumzile Mlambo-Ncguka amesema ni sahihi kabisa kwani usawa katika sekta zote utapunguza hata madhila yanayokumba jamii.

Akizungumza katika mahoajiano maalum na Dereck Mbatha wa Radio ya Umoja wa Mataifa, Bi. Mlambo-Ncguka ametolea mfano elimu akisema iwapo wanawake wengi zaidi wangalimaliza elimu ya sekondari, basi hata idadi ya vifo vya watoto wachanga ingalipungua kwa kuwa wangalikuwa na uwezo wa kulea watoto wao. halikadhalika kilimo..

(Sauti ya Phumzile)

"Iwapo wakulima wanawake wangalipatiwa kiwango sawia cha pembejeo; mbolea, mashine kwa kilimo idadi ya watu wasio na uhakika wa chakula ingalipungua kwa kwani watu wengi watakuwa na chakula kwa sababu uzalishaji wa chakula na kilimo utakuwa juu.”

Na kwa ajili ya mustakhbali bora kwa wanawake, Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UN-Women akawa na ujumbe kwa wasichana .

(Sauti ya Phumzile)

"Wasichana wakae shule zaidi, ni lazima wacheleweshe kupata watoto hadi pale watakapokuwa na uwezo wa kuwa nao na kuwatunza. Ni lazima wawe jasiri na wasiwe waoga kuzungumza kwani dunia ya leo ni mali yao kama ilivyo kwa wanaume.”

Katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani leo katika Umoja wa Mataifa kutakuwepo na tukio maalum amapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon anatarajiwa kuhutubia.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud