Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OPCW yapokea pendekezo la Syria kuhusu uondoshaji wa kemikali nje ya nchi hiyo

OPCW yapokea pendekezo la Syria kuhusu uondoshaji wa kemikali nje ya nchi hiyo

Serikali ya Syria imewasilisha pendekezo jipya lenye lengo la kuhakikisha uondoshaji wa kemikali zenye sumu nje ya nchi hiyo unakamilika kabla ya mwisho wa mwezi ujao wa Aprili.

Shirika la kimataifa la kupinga silaha za kemikali, OPCW limepokea pendekezo hilo likiitaka Syria kuhakikisha linazingatia muda kwani awali kemikali hizo za sumu zilitakiwa ziwe zimeshaondolewa nchini humo tarehe Tano Februari mwaka huu.

Mkurugenzi Mkuu wa OPCW Ahmet Üzümcü ameliambia baraza tendaji la shirika hilo kuwa jopo la pamoja la kuteketeza mpango wa silaha za kemikali za Syria tayari limethibitisha kuwa shehena nyingine mbili zimeondoka bandari ya Latakia. Amesema shehena nyingine inatarajiwa kufika bandari hiyo wiki hii na hivyo kufanya shehena zinazosafirishwa nje kufikia Sita.

Bwana Üzümcü amesema kiwango hicho ni asilimia 35 ya kemikali zote zinazopaswa kuondolewa Syria kwa ajili ya uteketezaji nje ya nchi. Amesema kwa sasa Syria ina vifaa vyote vinavyohitajika kwa kuchagiza uondoshaji wa kemikali hizo ikiwemo vizibau vya watendaji vya kujikinga na kemikali sumu pamoja na makasha ya kuweka kemikali hizo.

Kwa mantiki hiyo amesema itakuwa vyema kwa mazingira ya sasa kuweka kasi mpya kuondoa kemikali hizo ikizingatiwa kuwa ratiba iko nyuma ya tarehe zilizokuwa zimepangwa awali.

Wakati huo huo Mratibu mkuu wa jopo la pamoja la Umoja wa Mataifa na OPCW kuhusu Syria Bi. Sigrid Kaag kesho atalihutubia baraza la usalama kuhusu hali ilipofikia sasa ya uteketezaji wa mpango huo.