UNHCR yataka usaidizi kwa wakimbizi wa CAR na Sudan Kusini uharakishwe
Zaidi ya watu Milioni Moja na Laki Nane wamekimbia makazi yao huko Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati kutokana na majanga yanayoendelea kwenye nchi zao, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR katika kile kinachoelezwa kuwa ni kiwango kikubwa zaidi cha ukimbizi barani Afrika katika miaka ya karibuni. Tupate taarifa.
UNHCR inasema wakimbizi wa ndani na wale waliosaka hifadhi nje ya nchi zao wanakabiliwa na hali ngumu wakati huu ambapo ukata unazidi kuzuia uwezo wa mashirika ya misaada kukidhi mahitaii ya kibinadamu yanayoongezeka kila uchao.
Mathalani linasema watoto 15 kutoka Jamhuri ya AFrika ya Kati mwishoni mwa wiki walifariki dunia kutokana na utapiamlo na limeonya kuwa wengi zaidi wanaweza kukumbwa na janga hilo kutokana na uhaba wa chakula nchini mwao.
Melissa Fleming ni msemaji wa UNHCR mjini Geneva:
“Tumeshabaini mahitaji na tunafahamu fedha zinazohitajika. Iwapo utaangalia Sudan Kusini kwa sasa kiasi cha dola bilioni Moja kinachohitajika hakijapatikana.Ni jambo la kusikitisha watoto 15 wamefariki dunia na hali hiyo iko katika nchi zote kutokana na kushindwa kuwafikia kwa sababu ya ukosefu wa usalama. UNHCR inaendelea kuhudumia maelfu ya wakimbizi wa Sudan nchini Sudan Kusini na tumeshuhudia baadhi ya wakimbizi wa ndani wakijaribu kukimbilia kwenye kambi hizo kwani wanahaha kusaka hifadhi.”
Maombi ya fedha ya UNHCR kwa ajili ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan Kusini bado hayajakidhiwa kwa kiasi kikubwa. Ombi la Jamhuri ya Afrika ya Kati ni dola Milioni 551 lakini wamepta asilimia Tisa tu ilhali kwa Sudan Kusini wamepokea dola Milioni 26 kati ya Bilioni Moja nukta Mbili Saba zilizoombwa.