Hatua za kijeshi hazina nafasi Ukraine: Wajumbe wa Baraza

3 Machi 2014

Hatua za kijeshi hazina nafasi kwenye utatuzi wa mzozo wa kisiasa unaoendelea nchini Ukraine! Hiyo ni moja ya kauli zilizotolewa na wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wa kikao cha wazi kuhusu hali inayoendelea nchini Ukraine wakati huu ambapo jitihada za kimataifa zinaendelea kusuluhisha mzozo huo.

Kikao hicho kiliongozwa na Rais wa baraza hilo kwa mwezi huu wa Machi Balozi Sylvie Lucas ambaye ni Mwakilishi wa kudumu wa Luxembourg kwenye Umoja wa Mataifa.

Kabla ya wajumbe kupatiwa fursa ya kutoa mitazamo yao, Naibu Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa masuala ya siasa, Oscar Fernandez Toranco aliwapatia muhtasari akisema hali ya Ukraine imeendelea kuzorota kila uchao tangu kikao cha dharura cha baraza siku tatu zilizopita.

(Sauti ya Toranco)

“Napenda kurejelea wito wa Katibu Mkuu wa kupunguza mvutano haraka iwezekanavyo. Kama Katibu Mkuu alivyosisitiza wito wake kwa viongozi wa kimataifa, sote tunawajibu wa kuweka juhudi zetu kutathmini na kupatia suluhu la kudumu kwa pamoja.”

Miongoni mwa waliochangia ni Profesa Joy Ogwu, Mwakilishi wa kudumu wa Nigeria kwenye Umoja wa Mataifa na mjumbe wa baraza yeye akasema kilichoanza kama maandamano ya kisiasa kimegeuka janga..

(sauti ya Profesa Ogwu)

“Hali ya sasa Ukraine hususani Crimea inawasilisha kitisho cha dhahiri kwa amani na usalama duniani. Tungependa kuona mvutano unamalizwa haraka na majibizano ya uchochezi yanakoma. Pande husika zizingatie mashauriano kama njia ya kumaliza mzozo na kuwezesha hali ya utulivu kurejea Ukraine.”

Wajumbe wameunga mkono hatua ya Katibu Mkuu kumtuma Naibu wake Jan Eliasson nchini Ukraine kwenda kujionea hali halisi huku.