Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO washambulia kituo cha ADF Kivu Kaskazini

MONUSCO washambulia kituo cha ADF Kivu Kaskazini

Vikosi vya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, MONUSCO vimeendelea na jukumu la kulinda raia kwa kusaka vikundi vilivyojihami Mashariki mwa nchi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York hii leo, Msemaji wa Umoja wa Mataifa Martin Nesirky ametaja harakati hizo kuwa ni pamoja na zile za mwishoni mwa wiki ambapo helikopta mbili za MONUSCO zilishambulia moja ya vituo vya waasi wa ADF kwenye mji wa Sahasitisa, jimbo la Kivu Kaskazini.

Amesema mashambulio hayo yalikuwa ni katika kusaidia jeshi la DRC huku akimkariri Mkuu wa MONUSCO Martin Kobler akisisitiza kuwa hatua hizo zina lengo moja tu la kuepusha matukio ya mara kwa mara ya vikundi vilivyojihami kushambulia raia.

Mkuu huyo wa MONUSCO amewataka waasi wote kujisalimisha na kujiunga kwenye kambi ambazo zinaendeshwa na Umoja wa Mataifa huku akisema Umoja wa Mataifa utafanya kila iwezalo kulinda raia.