UNAMID yatiwa hofu na ghasia kusini mwa Darfur

3 Machi 2014

Ujumbe wa Pamoja wa Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa kwenye eneo la Darfur, UNAMID, limeeleza kutiwa hofu na ripoti za kuongezeka machafuko kusini mwa Darfur Suda, katika kipindi cha siku chache zilizopita.

Machafuko hayo yameripotiwa kusababisha uteketezaji wa vijiji kadhaa na idadi kubwa ya watu kuhama makwao karibu na Um Gunya, yapata kilomita 50 kusini mashariki mwa Nyala.

UNAMID imepokea pia ripoti za uporaji, utekezaji nyumba, watu kuuawa, pamoja na kuwasili wakimbizi wapya katika kambi za wakimbizi wa ndani za Al Salam na Kalma.

Walinda amani wamejaribu kuyafikia maeneo yaloathiriwa mara kadhaa, lakini hawakuruhusiwa na mamlaka za eneo hilo.

UNAMID imetoa wito kwa mamlaka kuruhusu askari wake kuyafikia maeneo hayo bila vikwazo ili watekeleze wajibu wao wa kuwalinda raia, kama walivyoidhinishwa na AU, UM na kukubaliwa na serikali ya Sudan.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter