Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNRWA yapigwa jeki ya dola 759,000 kuwasaidia wakimbizi wa kambi ya Yarmouk

UNRWA yapigwa jeki ya dola 759,000 kuwasaidia wakimbizi wa kambi ya Yarmouk

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwasaidia Wakimbizi wa Palestina, UNRWA, limesaini makubaliano ya ufadhili wa misaada ya dharura yenye thamani ya dola 759,000 kutoka kwa Shirika la Kiislam la Misaada ya Dharura, IRW. Mchango huo wa IRW utasaidia kufadhili utoaji misaada ya chakula na bidhaa za kujisafi kwa zaidi ya wakimbizi 70,000 wa Kipalestina walionaswa kwenye kambi ya Yarmouk na maeneo mengine ya mji wa Damascus ambayo yanakabiliwa na hali ngumu kupindukia.

Hatua hiyo ya ukarimu ya IRW imetokea siku mbili tu baada ziara ta Kamishna Mkuu wa UNRWA Filippo Grandi kuzuru kambi ya Yarmouk, ambapo alijionea jinsi maelfu ya watu kwenye foleni wakitarajia kupata angaa msaada wa chakula. Amesema dalili za ukosefu na utapia mlo ulokithiri miongoni mwa watu hao ambao walifanya safari ya kwenda kwa kituo cha ugawaji chakula licha ya hatari ya kupigwa risasi na walenga shabaha, zilionyesha haja ya kuwepo misaada ya chakula kutegemewa.

Mashirika ya IRW na UNRWA kwa pamoja yameelezea kuhofia hatma ya wakimbizi hao wa Palestina kwenye kambi ya Yarmouk na nyinginezo za muda katika eneo la Damascus, ambao wamekuwa wakilazimika kuhamahama katika kipindi cha miaka mitatu ya machafuko nchini Syria. Yamesema wakimbizi wa Palestina wamo hasa hatarini zaidi.