UM yajitolea kusuluhisha mzozo wa kisiasa Ukraine

3 Machi 2014

Umoja wa Mataifa uko tayari kutoa usaidizi wowote utakaowezesha kusuluhisha mzozo wa kisiasa unaoendelea nchini Ukraine, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon mjini Geneva, Uswisi wakati akizungumza na waandishi wa habari kama anavyoripoti Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Bwana Ban ambaye anatarajia kuwa na mazungumzo na Waziri wa Mambo ya nje wa Urusi, Sergei Lavrov ametaka kurejeshwa kwa amani Ukraine huku akiishi Urusi kujizuia kufanya kitendo chochote kinachoweza kuchochea mzozo huo. Ametaka uhuru, mamlaka na utawala wa Ukraine kuheshimiwa.

(Sauti ya Ban)

Tutajadili jinsi Umoja wa Mataifa unaweza kushirikiana na Urusi na mamlaka za Ukraine pamoja na wadau wengine ukiwemo Muungano wa Ulaya kuepusha mzozo zaidi na pia kuona jinsi ya kuendeleza mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine. Nilipozungumza kwa simu na Rais Putin siku ya Jumamosi nilimsihi ashughulikie jambo hili kwa kuhusisha moja kwa moja mamlaka za Ukraine. Jambo bora zaidi kwanza ni kumaliza mvutano. Ni muhimu pande zote zikatulia, zikaepuka kurushiana maneno na badala yake zifanye mashauriano.”

Hata hivyo katika hotuba yake kwa Baraza la Haki za binadamu, Bwana Lavrov amekanusha ripoti za jeshi la Urusi kuvamia Ukraine kwa kutuma askari eneo la Crimea. Badala yake majeshi yake yatakuwepo eneo hilo hadi utulivu wa kisiasa unarejea Ukraine.

(Sauti ya Lavrov)

“Hili ni suala la kulinda raia na rafiki zetu na kuhakikisah haki za binadamu hususan ile ya kuishi. Wale wanaojaribu kutafsiri hali hii kama uvamizi na kushia vikwazo au kususa, hao ni wale wale wadau wetu ambao wamekuwa wakisihi pande zao za kisiasa kukataa mashauriano na hatimaye wameigawa Ukraine. Tunawasihi waonyeshe uwajibikaji wao kwa kuweka kando siasa za kimaeneo na badala yake waweke mbele maslahi ya wananchi wa Ukraine mbele.

Tayari Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson, yuko Ukraien kwa mashauriano na mamlaka za nchi hiyo.