Hali ya usalama Ukraine yazorota; Ban azungumza na Putin

1 Machi 2014

Hali ya usalama nchini Ukraine inazidi kuzorota na kumtia wasiwasi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon na tayari amezungumza na Rais Vladmir Putin wa Urusi kuhusiana na suala hilo.

Hayo yamesemwa na msemaji wa Umoja wa Mataifa Martin Nesirky alipozungumza na waandishi wa habari mjini New York, wakati huu ambapo Robert Serry ambaye ni mjumbe wa Bwana Ban ameshindwa kwenda nchini Ukraine kwenye jimbo linalojitawala Crimea kutokana na sababu za kiusalama.

Nesirky amesema Katibu Mkuu amerejelea wito wake wa pande husika kuheshimu na kulinda uhuru, utaifa na mamlaka ya Ukraine huku akitaka utulivu kurejeshwa kwa mashauriano ya moja kwa moja kati ya pande hizo. Alipoulizwa kuhusu uamuzi wa bunge la Urusi juu ya kupeleka majeshi nchini Ukraine, Bwana Nesirky alisema..

Tumeona hizi taarifa lakini hatuna ufafanuzi wowote kwa sasa. Kwa wakati huu jambo muhimu hapa ni kurejesha utulivu na mazungumzo ya moja kwa  moja. Tunachohitaji sasa ni pande zote kuwa na utulivu na umakini kwenye kushughulikia jambo hili.”

Tayari Bwana Serry ametoa taarifa yake kuhusu kuahirisha ziara yake Crimea na kwamba sasa anakwenda Geneva, Uswisi ambako atampatia Katibu Mkuu Ban Ki-Moon muhtasari wa kile alichoshuhudia Ukraine. Bwana Ban anakwenda Geneva kwa ziara ya kikazi.

Wakati huo huo Baraza la usalama linafanya kikao cha dharura kuhusu Ukraine ambapo Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson atawapatia wajumbe muhtasari kuhusu hali ilivyo nchini humo.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter