Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lalaani shambulio Somalia

Baraza la Usalama lalaani shambulio Somalia

Shambulio lingine la kigaidi limefanyika hii leo kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishu na kusababisha vifo vya watu na majeruhi kadhaa ambapo wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wametoa taarifa kushutumu kitendo hicho na vinginevyo vya aina hiyo.

Tayari kikundi cha kigaidi cha Al Qaeda kimekiri kuhusika nalo huku wajumbe hao wa baraza wakirejelea mshikamano wao na wananchi na serikali ya Somalia katika kipindi hiki kigumu.

Wametuma rambirambi kwa familia za wafiwa na kuwatakia ahueni ya haraka majeruhi na kusisitiza azma yao ya kupinga aina zote za ugaidi kwa kuzingatia wajibu wa baraza hilo kwenye katiba inayounda Umoja wa Mataifa.

Wamesema hakuna kitendo au lengo lolote lile linaloweza kuhalalisha ugaidi na wametaka wahusika wafikishwe mbele ya sheria na kuelezea azma yao ya kuendelea kusaidia jitihada za kimataifa kutokomeza kitisho cha Al Qaeda.